Jumatano 18 Novemba 2026 - 20:30
Baraza Kuu la Hawza Nchini Iran, Latoa Salamu za Rambirambi Kufuatia Kifo cha Ayatullah Al-Udhma Wahid Khorasani

Hawza/ Baraza Kuu la Hawza limetoa salamu za rambirambi kupitia ujumbe maalumu kufuatia kifo cha Marji' mwenye hadhi kubwa, Ayatullah Hussein Wahid Khorasani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ifuatayo ni nakala ya ujumbe wa rambirambi uliotolewa na Baraza Kuu la Hawza kufuatia kifo cha Marji' mwenye hadhi ya juu, Ayatullah Al-Udhma Haji Sheikh Hussein Wahid Khorasani (Mwenyezi Mungu amrehemu).

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

Imepokewa kutoka kwa Imam Jaafar Swadiq (amani iwe juu yake), kwamba amesema:

“Muumini Faqihi anapofariki dunia, hutokea pengo kubwa katika Uislamu pengo ambalo hakuna kitu kinachoweza kuliziba.”

Kufariki Faqihi wa Ahlul-Bayt  (amani iwe juu yao), Marji' mwenye hadhi kubwa katika ulimwengu wa Kishia na mtetezi wa heshima na utukufu wa Uimamu na Wilaya, Ayatullah Al-Udhma Haji Sheikh Hussein Wahid Khorasani (Mwenyezi Mungu amridhie), ni msiba mkubwa na huzuni nzito kwa Hawza na wapenzi wote wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao).

Faqihi huyo mchamungu, ambaye katika miongo ya hivi karibuni alikuwa akihesabiwa miongoni mwa nguzo imara na adimu za elimu na umahiri katika Fiqhi, alitumia maisha yake yenye nuru katika juhudi endelevu za kielimu, kulea na kuandaa idadi kubwa ya wanazuoni wenye fadhila, kueneza na kusambaza mafundisho ya madhehebu safi ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), pamoja na kukabiliana na mitazamo potovu na upotofu katika nyanja hizo.

Kujitenga na anasa za dunia na kuishi maisha ya zuhdi na uchamungu, ikhlasi, mapenzi ya dhati na kujifungamanisha kwa kina na Maimamu watoharifu (amani iwe juu yao), hususan Bibi Fatimah Zahraa (amani iwe juu yake), kuhifadhi kwa umakini na usahihi urithi mkubwa na wenye thamani wa elimu ya Fiqhi, kutoa mwanga wa kielimu na kimalezi, kupambana na utawala wa Kitaghuti, kuunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu na kushiriki katika medani za mapambano ya haki dhidi ya batili, ni miongoni mwa sifa za kipekee za mwanachuoni huyo wa kimungu.

Baraza Kuu la Hawza za Kielimu, huku likitoa salamu zake za rambirambi, linatoa pole kutokana na pengo hili kubwa kwa Mtukufu Baqiyyatullah Al-A'dham (roho zetu ziwe fidia kwake), Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Maraji' wakubwa wa Taqalidi (Mwenyezi Mungu awadumishe katika utukufu wao), Hawza za kielimu, wanafunzi wake, wafuasi wake katika masuala ya Taqalidi, wapenzi na wafuasi wa Marji' huyo, na hususan familia yake tukufu, watoto wake waheshimiwa pamoja na ndugu na jamaa zake wote.

Vilevile, Baraza linamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amnyanyulie Faqihi huyo wa kimungu daraja za juu kabisa, na awajaalie ndugu na jamaa zake waliobaki subira njema na malipo makubwa.

Baraza Kuu la Hawza za Kielimu Nchini Iran

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha